Thursday, May 24, 2012

HESLB NA HAZINA KOMESHENI UZEMBE HUU

HESLB na Hazina sasa komesheni udhaifu

Umekuwa ni kama ugonjwa wa kudumu mwaka baada ya mwaka, wanafunzi wa elimu ya juu ni lazima wagome kutokana na ama kukwama kwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) au kulalamikia utaratibu wa kutathminiwa ambao uamua mwanafunzi akopeshwe kwa kiwango gani kuanzia asilimia 20 hadi 100.

Tunaweza kusema kuwa kwa sasa kuna utamduni wa migomo katika vyuo vya elimu ya juu katika kudai mikopo yao. Hata wanafunzi wenyewe wa elimu ya juu wanalijua hilo ndiyo maana wengi wamesikika wakisema kuwa wanagoma ili fedha zao zitolewe.

Ni ada kugoma ili fedha za mikopo zitolewe. Na kweli kila wanafunzi hawa wanapogoma basi hazipiti siku mbili watu watakimbizana huko na huko na hatimaye fedha zitafikishwa ama kwenye akaunti zao moja kwa moja au hata vyuoni kwao.
Itakumbukwa kwamba mwaka juzi mwishoni vyuo vya elimu ya juu vilichelewa kufunguliwa kwa sababu ya madai kwamba mchakato wa kuweka mambo sawa ulikuwa ukiendelea ikiwa ni pamoja kuepuka migogoro ya kila wakati kwamba wanafunzi wanafika vyuoni lakini kunakuwa hakuna fedha kutoka Bodi ya Mikopo.

Kuchelewa kufunguliwa kwa vyuo hivyo mwaka juzi kulizua malumbano ya kisiasa yakijielekeza kwenye hisia kwamba wanafunzi wapatao 60,000 hivi wa vyuo hivyo wangekosa haki yao ya kupiga kura; huku wengi wakienda mbali zaidi na kudai kwamba zilikuwa ni njama za kupunguza kura za baadhi ya wagombea.

Vyombo mbalimbali vya kiserikali vilivyotoa kauli kuhusu hilo vilisisitiza juu ya kuchelewa kufunguliwa huko kuwa kulitokana na ulazima wa kukamilisha taratibu muhimu za kudahili wanafunzi, lakini pia kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanikiwa kabla ya vyuo hivyo kufunguliwa.

Ni jambo la ajabu kuona kwamba kumbe hata baada ya kuchelewa kufungua vyuo kwa kiasi hicho, bado mikopo ya wanafunzi haijashughulikiwa ipasavyo kiasi cha kuwa chanzo cha migomo.

Wanafunzi wa Mkwawa kipindi fulani waliozungumza na kusema kuwa walikuwa wamekaa kwa siku tatu bila chakula kwa sababu mikopo yao kutoka Bodi ya Mikopo ilikuwa haijatolewa.

Tunasikitika kwamba hali hii inawapata wanafunzi ambao wanalazimika kukatiza masomo na kuingia katika mapambano na dola ili kupata haki yao. Ni jambo baya na ambalo hakika halistahili kuungwa mkono kwamba uzembe unaruhusiwa kuota mizizi katika utekelezaji wa majukumu wa watumishi wa umma kiasi cha kuwafanya wajenge utamaduni wa kudai haki kwa migomo mwaka baada ya mwaka.

Tunaamini kwamba HESLB wanajua fika kwamba vyuo vinafunguliwa lini, wanajua wanafunzi walio na sifa za kupewa mikopo ni wangapi ni nani, lakini pia wanajua fika kwamba ulipaji wa fedha kutoka benki moja hadi nyingine hapa nchini huchukua muda gani, ili kwa kuzingatia hayo yote wahakikishe kwamba malipo ya wanafunzi yanawafikia kwa wakati.

Kama kikwazo ni Hazina, kwa maana ya kutoa fedha kwenda HESLB nako hali ni hiyo hiyo, wanajua wanafunzi wanahitaji kula, wana gharama nyingine tu za kulipa na kipato pekee na cha hakika kwa wale walio na sifa ya kukopeshwa ni mkopo husika ambao hulipwa kwa utaratibu mahususi uliokubalika, aghalab kila mwezi.

Kwa maana hiyo, hakuna asiyejua umuhimu wa kuwajengea wanafunzi hawa mazingira mazuri ya kusoma ikiwa ni pamoja na kuwahakikisha kwamba wanalipwa fedha zao kwa wakati ili isiwe sababu ya kuvuruga taratibu nyingine za masomo.

Kila tunapoona hali ya migomo katika vyuo vya elimu ya juu ikijirudia mwaka baada ya mwaka sababu zikiwa ni zile zile, yaani kucheleweshwa kwa mikopo ya wanafunzi kutoka HESLB tunaanza kujawa na hofu kwamba huenda wapo wanaonufaika na hali hii, vinginevyo kwa nini haikomeshwi?

Tunafikiri wakati umefika sasa HESLB au Hazina kujisafisha na lawama hizi kwa kuwawajibisha wote wanaosababisha usumbufu huu ambao kimsingi unalea nautamaduni wa migomo vyuoni. Sisi tunasema hali hii haikubaliki.  kukuza

No comments:

Post a Comment