MIMBA MASHULENI BADO NI TATIZO!
Wengi huchanganyikiwa
Tatizo la mimba masuleni si geni sana kwetu, ni tatizo lililokuwepo na lipo na linaendelea kuwepo japokuwa wanasiasa na wanaharakati kadhaa wanaendelea kulipigia kelele.Binafsi katika kusoma kwangu kuanzia shule ya msingi mpaka nilipomaliza kidato cha sita nimeshuhudia wasichana wengi wakishindwa kuendela na masomo kwa kupata ujauzito, Hapa nazungumzia wasichana niliosoma nao aidha darasa moja au shule moja kwa ujumla wake, achilia mbali wale waliofanikiwa kutoa na kuendelea na masomo, hapa nazungumzia wale walioshindwa kabisa kuendelea na masomo na ndoto zao kutoweka kwa kuporwa mustakabali wa maisha yao na wanaume wakware.Tatizo la mimba mashuleni limekuwa ni sugu kuanzia shule za msingi, sekondari mpaka vyuoni kote huko hapafai. Yaani ni jambo la kawaida kabisa kusikia kuwa mwanafunzi fulani ana mimba ya mtu asiyemfahamu.
Kila mwaka kuna maelfu ya mabinti wa shule wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata mimba na hili sio tatizo la hapa nchini peke yake bali ni tatizo la bara la afrika, kwani ukiingia mtandaoni na kusoma takwimu kutoka vyanzo mbalimbali vya habari katika nchi nyingi za Afrika utakutana na mambo ya kutisha humo, kuna wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kujazwa mimba.Hili tatizo sio tu linawasikitisha wazazi waliotumia fedha zao nyingi katika kumsomesha binti husika aliyepata ujauzito bali pia wanakuwa wameongezewa mzigo wa malezi ya mtoto asiyejulikana ni wa nani. Hii huwakatisha tamaa sana wazazi na ndio sababu wazazi wengi wanahofu ya kuwaendeleza watoto wao wa kike na elimu ya sekondari kwa kuhofia kupoteza muda na fedha zao bure. Kama tulivyoona kwa baba yake Anita alipokataa kumuendeleza mwanae na kutaka kumuoza kwa kile alichodai kuwa watoto wa kike hata wakisomeshwa hawainufaishi familia husika na badala yake hunufaisha familia ya wakwe zake, ingawa haikuwa hivyo kwa Anita, lakini mzee yule hatajiona kuwa alikuwa sahihi kwa kiasi fulani kutokana na binti huyo kupata ujauzito akiwa tu ndio ameingia kidato cha pili?
Hebu tuangalie sababu ambazo zinachangia wanafunzi kupata ujauzito:Kwa kawaida mtoto yeyote wa kike akishafikisha umri wa kuanzia miaka 9 mpaka 12 anashuhudia mabadiliko katika mwili wake ikiwa ni pamoja na kuziona siku zake, hapa ndipo wazazi wanapopaswa kuzungumza na mabinti zao na kuwaelimisha juu ya kuyapokea mabadiliko hayo na namna ya kupambana na vishawishi vya wanaume na bila kusahau kuwaeleza ukweli kuhusu uwezekano wa kupata ujauzito iwapo watashiriki kufanya ngono. Namshukuru mama yetu alikuwa ni muwazi sana kwetu kiasi kwamba mimi na dada zangu tumemudu kuvuka hizo changamoto mpaka tumeweza kumaliza shule na wengine mpaka vyuoni.Kama inavyotokea kwa mabinti na ndivyo inavyotokea kwa wavulana, nao wanapofikisha umri wa kubalehe hushuhudia mabadiliko kadhaa katika miili yao.
Wazazi wengi hawawajibiki katika kuwaelimisha mabinti zao na badala yake jukumu hilo wanawaachia waalimu ambao nao wanayo majukumu mengi ya kuandaa masomo na kufundisha,na hivyo maisha ya mabinti hao huwekwa rehani kwa wanaume wakware wenye ndimi zenye asali.
Mabinti
wengi wamejikuta wakipata ujauzito kutokana na kutojua kuwa kucheza na
wanaume ni sawa na kucheza na moto, na hiyo inatokana na kutopata elimu
juu ya mabadiliko ya mwili na hisia za kimapenzi wanapokuwa wamevunja
ungo kutoka kwa wazazi wao.
No comments:
Post a Comment