NCHINI Tanzania, kila mwaka zaidi ya wasichana 8,000 huacha shule kutokana na mimba (Takwimu za Umoja wa Mataifa kwa Tanzania Julai 2010).
Hawa ni wale wanaoacha shule moja kwa moja, lakini wapo wengine kwa maelfu wanaoripotiwa kuwa ni watoro, kumbe hawako shule kwa sababu wakipata mimba hawarudi shule kwa kuhofia kufukuzwa.
Takwimu myingine za hivi karibuni zinaonyesha kwamba idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kutokana na mimba imeongezeka hasa katika mwaka wa 2008-2009 (MoEVT 2008 & BEST 2010). Japo wengi wao wanaripotiwa kuwa ni watoro, ni wazi kwamba mimba za utotoni ndiyo sababu kuu za utoro huo.
Katika shule za msingi waliokatisha masomo kwa sababu ya mimba ni 1,056 (BEST 2011 uk 31). Bado taarifa za Utafiti kuhusu mimba za utotoni kwa wasichana uliofanywa mwaka 2010 na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), zinatoa picha ya kutisha ya tatizo hili. Je chanzo chake nini?
Moja, hali duni ya uchumi wa familia. Ufukara na hali ngumu ya kiuchumi ya familia ni kisababishi kikubwa cha wasichana kukatisha masomo.
Hali ngumu ya kiuchumi katika familia inasababisha yafuatayo: Wazazi wanashindwa kuwatimizia watoto wa kike mahitaji yao ya msingi ya kimasomo, hivyo watoto wa kike wanakua wahitaji muda wote kiasi cha kuathirika kisaikolojia.
Baadhi wanaamua kuacha shule na kubaki nyumbani ama kuolewa ili angalau wapambane na maisha wakiwa nje ya mfumo wa shule.
Pili, uduni wa elimu inayotolewa na mazingira magumu ya kujifunzia ni sababu kubwa inayofanya wasichana wakatishe masomo yao. Shule binafsi zenye mazingira mazuri hata zikiwa kijijini, watoto wengi hufanikiwa kumaliza shule na kunufaika nayo.
Kama elimu inayotolewa hairidhishi, mtalaa haushabihiani na mahitaji ya wanafunzi kimaisha au hauonyeshi dalili za kuwanufaisha wanafunzi maishani, wanafunzi hukata tamaa na wazazi wanasita kusomesha watoto wao kwenye shule dhaifu.
Tatu, malezi duni ya wazazi na tamaa za wasichana wenyewe. Jambo hili limetajwa na wazazi na wasichana wenyewe tuliofanya nao mahojiano katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Baadhi ya wazazi hawatumii muda mwingi kuwajenga watoto wao kimakuzi na kimaadili. Hivyo wasichana waliokosa maadili wanashindwa kujimudu, wanaiga na kufuata ushawishi mbaya.
Nukuu hii ya mwanafunzi mmoja niliyezungumza naye inathibitisha hili. Mimi ninavyoona ni tamaa za mwili, tunapofikia ule umri wa kupevuka tunakuwa na mihemko katika mwili ambayo usipojizuia utajikuta unapata ujauzito katika umri mdogo. Lakini yanazuilika kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwa bize na masomo na kufanya mazoezi.
Nne, kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi. Wasichana waliopevuka kimaumbile wanahitaji elimu ya uzazi ili wayapokee mabadiliko ya makuzi kwa umakini.
Lakini inaonekana wazazi wengi hasa wa maeneo ya vijijini, hawaongei na watoto wao wa kike ambao wako kwenye umri wa kukua. Bila wasichana kupewa maelekezo ya msingi kuhusu ukuaji wao na hasa namna ya kuepukana na mimba, wengi hudumbukia kwenye mimba za utotoni bila kujua.
Tano, mitazamo kuwa thamani ya wasichana ni kuolewaa au kuwa mama. Hiki ni chanzo kikubwa cha tatizo la mimba za utotoni. Bado kuna wanajamiii wenye mtazamo kuwa mtoto wa kike thamani yake ni kuolewa ama kuzaa na kuwa mama.
Wenye mitazamo hii ndio wanaowakatisha tamaa wasichana kusoma na kushiriki kwenye vitendo vya kuwavurugia maisha. Utafiti wa masuala ya afya uliofanywa na Serikali na wadau, unabainisha ukweli huu ambao bado unaathiri jamii nyingi za Kitanzania (TDHS 2004/05).
Saba, mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii na uduni wa sheria zetu ni chanzo kingine kikubwa. Hili liko kuanzia kwa wazazi hadi walimu shuleni wanaoshiriki kuwapa mimba wanafunzi.
Fikiria, mwalimu ndiye anayepewa dhamana ya kumlea mtoto na anabeba majukumu yote; ulezi, kuwa mzazi na pia kufundisha, hivyo huyu ni baba. Sasa baba kumpa mimba mtoto ni mwiko na fedheha kubwa katika familia ambayo ni shule na jamii.
Wapo pia wafanyakazi wa Serikali na taasisi mbalimbali ambao wana dhamana ya kuwaendeleza watoto wetu lakini nao wanachangia kuwapa mimba watoto wetu.
Nane, ni sisi wazazi na pamoja na Serikali zetu tunaoshindwa kuthibiti tatizo hili kwani tumeiacha jamii ifanye inavyotaka juu ya watoto wetu wa kike na wa kiume. Wasichana wanabakwa na wavulana wanalawitiwa.
Hakuna malezi wala ulinzi wowote kutoka kwa wananchi na Serikali. Tofauti ni kwamba wavulana wao hawapati mimba, lakini wote tumewaaacha bila malezi ya kitaifa-wanalelewa na makundi rika, runinga, michezo ya kuigiza, kumbi za starehe na matamasha ya kijamii.
Kupata mimba si kwa sababu wamevaa nguo fupi ama wana kiherehere, bali ni tamaa mbaya na ulafi mchafu wa baadhi ya wanaume husika wanaowapa mimba baada ya kushindwa kuzishinda tamaa zao ama kwa imani potofu.
Ni wajibu wa taifa kukemea vitendo hivi, kutoa elimu ya kutosha kwa watoto na jamii kuhusu athari za mwenendo kwa maisha ya watoto wetu wa kike ambao ni nguvu kazi muhimu ya taifa letu.
No comments:
Post a Comment