
George Kayala na Haruni SanchawaTUKIO la mwanamke Rehema Nungu kukutwa ameteketea kwa moto ndani ya gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 883 BLA katika msitu wa Mabwepande, jijini Dar Agosti 1, 2012 linazidi kugusa akili za wengi hasa kutokana na utata wa tukio lenyewe na hii ndiyo ripoti kamili.
Taarifa zilizopenyezwa na ndugu mmoja wa Simon Sakilu ambaye ni mume wa marehemu, zinadai kuwa kabla ya tukio hilo, Rehema na mumewe walikuwa kwenye ugomvi mzito usiokuwa na dalili ya kumalizika.
Habari zinadai kwamba marehemu alikuwa akidaiwa fedha na mfanyabiashara mmoja (hakutajwa jina) lakini mumewe hakulijua deni hilo mpaka siku za mwisho za uhai wa Rehema ambapo hata hivyo hakumuuliza.
Aidha, ikadaiwa kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa akimdai marehemu kwa vitisho kwamba asipolipa atamwambia mumewe, jambo ambalo mwanamke huyo hakutaka litokee.
Siku ya tukio, habari zinadai kuwa marehemu aliamka mapema na kufanya shughuli za nyumbani na baada ya muda inadaiwa alikunywa sumu ambayo haikujulikana ni ya aina gani.
Ikazidi kudaiwa kuwa baada ya kitendo hicho, mumewe alifanya juhudi za kumnywesha maziwa ili kuokoa uhai wake lakini ilishindikana kufuatia mke kumzidi nguvu mumewe na kukimbilia kwenye gari na kuondoka nyumbani kwenda kusikojulikana.
“Mwanamke alipokunywa sumu, mumewe (Simon)alifanya juhudi za kumpa maziwa ili kuokoa maisha yake lakini alizidiwa nguvu, mke akatoka na gari na kwenda kusikojulikana.
“Simon alikwenda kukutana na mdai wa mkewe na kumlipa fedha zake akiamini mkewe alikunywa sumu kwa sababu ya deni, baada ya malipo akampigia simu mkewe ili kumtaarifu lakini simu hiyo ilikuwa inaita na kukatika, baadaye haikupatikana kabisa,” alisema ndugu huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake gazetini.
Kuanzia hapo, ndugu walianza kumsaka Rehema mpaka Agosti 2 mwaka huu habari zilipopatikana habari kwamba kuna gari limekutwa limeteketea kwa moto kwenye msitu wa Mabwepande. Mtu aliyedaiwa ndiye alikuwa dereva naye alikuwa ameungua na kubaki majivu na fuvu likiwa sehemu ya kiti.
Hata hivyo, ndugu hawakutaka kuweka msiba wakiamini aliyefariki dunia kwa moto huo anaweza asiwe Rehema. Ili kujiridhisha na hilo, walichukua mabaki hayo na kuyapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa vipimo vya DNA.
MUME ANA SIRI NZITO?
Habari zaidi kutoka ndani ya familia hiyo zinadai kuwa huenda Simon ana siri nzito juu ya kifo cha mkewe Rehema kwani haingii akilini mume kuzidiwa nguvu na mkewe wakati wa kumsaidia kumnywesha maziwa.
Aidha, mpenyesha habari huyo aliendelea kufunguka kwamba ilikuwa ni kawaida kwa wanandoa hao kutibuana na mke kwenda anakojua hata kwa siku tatu bila mwanaume kujishughulisha kumtafuta.
MAELEZO UPANDE WA MKE
Agosti 6, 2012 mapaparazi wetu walifika nyumbani kwa marehemu Rehema, Mbezi Beach, Dar na kukuta watu wachache ikidaiwa hali hiyo ilitokana na wengi kutoamini kama Rehema alifariki dunia. Mume wa marehemu hakuwepo msibani hapo bila kujulikana alikokwenda.
Alipotafutwa ndugu wa marehemu kuzungumzia suala hilo, kila mmoja aliruka na kudai mwenye uwezo wa kuzungumzia jambo hilo ni mama mzazi ambaye naye aligoma kusema lolote.
“Mwenye uwezo wa kuzungumzia suala hilo ni mama mzazi lakini amegoma kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa vile anahisi kuna mchezo mchafu umefanyika,” alisema ndugu mmoja.
Hata hivyo, mtu mmoja wa karibu na familia ya marehemu alisema kuwa habari kamili juu ya msiba huo zitapatikana mara baada ya kupata vipimo kutoka kwa mkemia mkuu kubaini kama kweli aliyekutwa ameteketea kwa moto ndani ya gari ni Rehema.
“Ni vigumu kulizungumzia suala hili kwani linatatanisha, unaweza kusema aliyekufa ni Rehema na matokeo ya mkemia mkuu yakitoka yakaonesha tofauti, inaweza kuleta shida, tusubiri majibu kwanza,” alisema mtu huyo bila kutaja jina lake.
No comments:
Post a Comment