MWANAFUNZI wa darasa la saba Shule ya
Msingi Hogolo, wa umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa) ambaye ni Mkazi
wa Mtaa wa Ikulu Kijiji cha Hogolo wilayani Kongwa, mkoani Dodoma
ameuawa kwa kunyongwa na kuzikwa kwenye shimo nyuma ya nyumba yao karibu
na choo baada ya kubakwa.
Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa
chanzo cha mauaji hayo yaliyofanyika Jumamosi iliyopita ni wivu wa
kimapenzi kwani marehemu enzi za uhai wake, anadaiwa alikuwa amevunja
uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu, Heri Aboubakar na kuanzisha
uhusiano mpya na Wilfredy Muhaha maarufu Kabo.
Hata hivyo bado haijafahamika
muuaji halisi wa marehemu huyo licha ya polisi kuwashikilia watu kadhaa
kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo akiwemo mpenzi wake wa sasa,
Muhaha.
Mbali na Muhaha wengine
wanaoshikiliwa Polisi ni Ashad Jafari ambaye ni mkulima na mkazi wa Mtaa
wa Nyerere Hogolo ambaye ni rafiki wa marehemu na Rino Mazoea, mkulima
na mkazi wa Ikulu Hogolo wilayani Kongwa ambaye ni kaka wa marehemu.
Kamanda Zelothe Steven alisema
wanamtafuta Aboubakar ambaye amekimbia kijijini hapo na hajulikani alipo
mpaka sasa. Katika tukio hilo, kaka wa marehemu ambaye pia anashikiliwa
Polisi, katika maelezo yake ya awali alidai kusikia purukushani
zikitokea usiku wa tukio hilo la mauaji lakini hakutoka usiku huo
kushuhudia nini kinaendelea.
Marehemu alikuwa akiishi na babu
na bibi yake hapo kijijini na siku ya tukio , walezi hao, walikuwa
wameondoka kwenda katika vijiji vya jirani, ambapo bibi yake alikuwa
amekwenda Kongwa kwa ajili ya kujengea makaburi na babu yake alikwenda
Kijiji cha Banyi Banyi kutembelea wagonjwa.
chanzo ni www.habarileo.co.tz
No comments:
Post a Comment